Pages

Thursday, December 25, 2014

Hadithi ya Yesu kwenye Qur'an

Hadithi ya Yesu ni moja ya hadithi ndefu sana kwenye Qur'an, ilibidi aongelewe zaidi ya ukurasa moja. Qur'an ilianza na mababu zake, familia ya Imran, mpaka kwa mama yake Mariam ikaishia kwake. Unapata na stori kidogo ya John the Baptist mwanzo wake. Hapa nimeku wekea mkusanyiko wa hadithi yake kutoka Suratul Al-Imran(Familia ya Imran), ukurasa wa 3 kwenye Qur'an aya 33-60, iliyo tafsiriwa na Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani, mwenyezi Mungu amrehemu.


Kuzaliwa kwa Mariam

Hakika Mwenyezi Mungu alimteuwa Adam na Nuhu na ukoo wa Ibrahim na ukoo wa Imran juu ya walimwengu wote.Ni wazao wao kwa wao; na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia na Mwenye kujua. Alipo sema mke wa Imran: Mola wangu Mlezi! Nimekuwekea nadhiri kilichomo tumboni mwangu kuwa wakfu; basi nikubalie. Hakika Wewe ndiye Mwenye kusikia na Mwenye kujua. 

Basi alipo mzaa alisema: Mola wangu Mlezi! Nimemzaa mwanamke - na Mwenyezi Mungu anajua sana aliye mzaa - Na mwanamume si sawa na mwanamke. Na mimi nimemwita Maryamu. Nami namkinga kwako, yeye na uzao wake, uwalinde na Shet'ani aliye laaniwa.Tena Mola wake Mlezi akampokea kwa mapokeo mema na akamkuza makuzo mema, na akamfanya Zakariya awe mlezi wake.Kila mara Zakariya alipo ingia chumbani kwake alimkuta na vyakula. Basi alimwambia: Ewe Maryamu! Unavipata wapi hivi? Naye akasema: Hivi vinatoka kwa Mwenyezi Mungu; na Mwenyezi Mungu humruzuku amtakaye bila ya hisabu.

Pale pale Zakariya akamwomba Mola wake Mlezi, akasema: Mola wangu Mlezi! Nipe kutoka kwako uzao mwema. Wewe ndiye unaye sikia maombi.  Alipo kuwa kasimama chumbani akisali, Malaika kamnadia: Hakika Mwenyezi Mungu anakubashiria Yahya(John the Baptist), ataye kuwa mwenye kusadikisha neno litokalo kwa Mwenyezi Mungu, na ni bwana na mt'awa na Nabii kwa watu wema.Akasema Zakariya: Mola wangu Mlezi! Vipi nitapata mwana na hali ukongwe umenifikia, na mke wangu ni tasa? Akasema: Ndivyo vivyo hivyo, Mwenyezi Mungu hufanya apendavyo. Akasema: Mola wangu Mlezi! Niwekee alama. Akasema: Alama yako ni kuwa hutasema na watu kwa siku tatu, isipo kuwa kwa kuashiria tu. 

Na mdhukuru Mola Mlezi wako kwa wingi na mtakase jioni na asubuhi.Na angalia pale Malaika walipo sema: Ewe Maryamu! Kwa hakika Mwenyezi Mungu amekuteuwa, na akakutakasa, na akakutukuza kuliko wanawake wote.Ewe Maryamu! Mnyenyekee Mola Mlezi wako na usujudu na uiname pamoja na wainamao. Hizi ni khabari za ghaibu tunazo kufunulia; nawe hukuwa nao walipo kuwa wakitupa kalamu zao nani wao atamlea Maryamu, na hukuwa nao walipo kuwa wakishindana.


Kuzaliwa kwa Yesu

Na pale Malaika walipo sema: Ewe Maryamu! Hakika Mwenyezi Mungu anakubashiria (mwana) kwa neno litokalo kwake. Jina lake ni Masihi Isa mwana wa Maryamu, mwenye hishima katika dunia na Akhera, na miongoni mwa walio karibishwa (kwa Mwenyezi Mungu).Naye atazungumza na watu katika utoto wake na katika utuuzima wake, na atakuwa katika watu wema.Maryamu akasema: Mola wangu Mlezi! Vipi nitampata mwana na hali hajanigusa mwanaadamu? Mwenyezi Mungu akasema: Ndivyo vivyo hivyo, Mwenyezi Mungu huumba apendacho.Anapo hukumu jambo, huliambia: Kuwa! Likawa.



Na atamfunza kuandika na Hikima na Taurati na Injili.Na ni Mtume kwa Wana wa Israili kuwaambia: Mimi nimekujieni na Ishara kutoka kwa Mola Mlezi wenu, ya kwamba nakuundieni kwa udongo kama sura ya ndege. Kisha nampuliza anakuwa ndege kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na ninawaponesha vipofu wa tangu kuzaliwa na wakoma, na ninawafufua maiti kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, na ninakwambieni mnacho kila na mnacho weka akiba katika nyumba zenu. Hakika katika haya ipo Ishara kwenu ikiwi nyinyi ni wenye kuamini. Na ninasadikisha yaliyo kuwa kabla yangu katika Taurati, na ili nikuhalalishieni baadhi ya yale mlio harimishiwa, na nimekujieni na Ishara kutokana na Mola Mlezi wenu. Kwa hivyo mcheni Mwenyezi Mungu na nit'iini mimi.Hakika Mwenyezi Mungu ni Mola wangu Mlezi na ni Mola wenu Mlezi. Basi muabudni Yeye. Hii ndiyo Njia Iliyo Nyooka.

Isa alipo hisi kuwa kati yao pana ukafiri alisema: Nani wasaidizi wangu kwa Mwenyezi Mungu? Wanafunzi wake wakasema: Sisi ni wasaidizi wa Mwenyezi Mungu. Tumemuamini Mwenyezi Mungu, na shuhudia kwamba sisi hakika ni Waislamu.Mola wetu Mlezi! Tumeyaamini uliyo yateremsha, na tumemfuata huyu Mtume, basi tuandike pamoja na wanao shuhudia.Na Makafiri walipanga mipango na Mwenyezi Mungu akapanga mipango, na Mwenyezi Mungu ndiye mbora wa wenye kupanga.Pale Mwenyezi Mungu alipo sema: Ewe Isa! Mimi nitakutimizia muda wako wa kuishi(Hawatakuuwa hao maadui), na nitakunyanyua kwangu, na nitakutakasa na wale walio kufuru, na nitawaweka wale walio kufuata juu ya wale walio kufuru, mpaka Siku ya Kiyama. Kisha marejeo yenu yatakuwa kwangu, nikuhukumuni katika yale mliyo kuwa mkikhitalifiana.

Ama wale walio kufuru, nitawaadhibu adhabu kali katika dunia na Akhera, wala hawatapata wa kuwanusuru. Na ama wale walio amini na wakatenda mema basi Mwenyezi Mungu atawalipa ujira wao kaamili. Na Mwenyezi Mungu hawapendi madhaalimu.Haya tunayo kusomea ni katika Aya na Ukumbusho wenye hikima.Hakika mfano wa Isa kwa Mwenyezi Mungu ni kama mfano wa Adam; alimuumba kwa udongo kisha akamwambia: Kuwa! Basi akawa.Hii ni kweli itokayo kwa Mola wako Mlezi. Basi usiwe miongoni mwa wanao fanya shaka.

To get the english version of the same story, read my previous post here>>> 

No comments:

Post a Comment